Karismatiki Katoliki waombea waathirika tetemeko Kagera
WAUMINI wa Kanisa Katoliki kupitia mkondo wa Karismatiki Katoliki katika kanisa hilo Jimbo Kuu la Dar es Salaam wamewaombea faraja na kupona haraka majeraha waathirika wa tetemeko lililotokea Septemba 10 mkoani Kagera.
Aidha, katika maombi hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Kongamano la Roho Mtakatifu lililomalizaka jana, sadaka maalumu ya Sh milioni moja ilitolewa katika kuchangia waathirika hao ambayo itajumlishwa na sadaka nyingine zinazoendelea kutolewa na kanisa hilo nchini.
Akizungumza kueleza umuhimu wa kuombea Taifa amani na kuwaombea wengine wanapopata matatizo mbalimbali, mwongozaji wa Kongamano hilo, Selina Kolumbani, alisema kumtolea Mungu kwa kusaidia wahitaji ndiko kunakomgusa Mungu zaidi.
Kolumbani alisema pamoja na kuweka sadaka ya pili ya Kongamano Ijumaa iliyopita kuchangia waathirika hao wa tetemeko la Kagera, aliwataka waumini wenzake kujenga utamaduni wa kusaidia wengine wanapopata matatizo kuwa sehemu ya maisha.
Kongamano hilo lilianza Septemba 26 na kumalizika jana Oktoba 2, mwaka huu pia kulifanyika maombi maalumu ya kuliombea Taifa ambapo serikali iliwakilishwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Annastazia Wambura.
Akifafanua kuhusu umuhimu wa sadaka, Pascal Masenge alisema kumtolea Mungu kulikokamilika ni kule kunakobeba imani na sadaka yako, inabeba maombi ya mahitaji yako.
Comments
Post a Comment